Inapakia...
Inapakia...

Dr Brighton Shoo
Mwandishi na Mwenyekiti
“POMBE "Alcohol" Pombe sio kitu kipya kwa binadamu yeyote kutokana na matumizi yake makubwa Sana katika kila jamii. Pombe au alcohol kwa asili ni matokeo ya hatua za kuchacha kwa chakula. Ukiwa na chak…”
POMBE "Alcohol"
Mara nyingi utengenezaji wa pombe huusisha mchanganyiko wa sukari, maji, na mazingira yasiyo na oksijeni. Na hapo utapata pombe au alcohol Kama matokeo ya uvundaji. Kama utaruhusu sana oksijeni matokeo ya pombe itakayoundwa itabadilika zaidi na kuunda asidi.hii ndiyo maana utengenezaji wa pombe unahitaji taaluma nyingi za kubalansi kiwango Cha oksijeni, maji, sukari na hata mwanga.
Kwanini Chupa za Beer haziangazi?
Pombe nyingi kama Beer huwekwa kwenye chupa zisizoangaza, kahawia, kijani, au nyeusi, hii ni kubalansi Mwanga. Mionzi ya Mwanga wa Mchana, au wa Blue wenye mionzi ya 400 mpaka 550 hubadilisha kemikali zinazochochea hisia za kutulia unapokunywa pombe, za Humulones, kuwa Isohumulones ambazo huifanya kuwa Chachu sana. Pia Pombe nyingi za Chupa ikiwemo na Juisi za Energy huwekwa kwenye chupa zisizoangaza ili kutoziwaisha kuharibika, kutokana na tabia ya Mwanga kuharibu Vitamin C na kupelekea vitu kuwahi kuchacha. Rangi hizi za Chupa hufyonza mionzi ya Mwanga kuanzia asilimia 70 mpaka 100% na kuifanya pombe idumu zaidi.
Kiini Cha Pombe
Mara nyingi pombe nyingi Sana, huwa na kemikali maalumu zaidi inayoitwa "ethanol". Na kemikali zote za asili ya pombe, huwa na jina linaloishia neno "-ol". Mfano, methanol,isopropanolol n.k. lakini "-etol' au ethanol, ndiyo inayokubalika zaidi kwa matumizi ya pombe nyingi. Aina zingine za Pombe ni sumu kabisa kwa mwili. Mfano, methanol ambayo hata mwilini mwetu huzalishwa ukinywa soda au pipi zenye ‘’Aspartame’’, tuliona namna ilivyokuwa ikichangia sana kuudhuru ubongo. Hiyo isopropanol ndiyo hutumika kwenye ‘’sanitizer’’ za kuua vimelea na hata kuoshea injini. Ni ethanol tu ambayo ijapokuwa nayo ni sumu, ila mwili una uwezo wa kuivumilia kwa kiwango chake huku ukiathirika.
Pombe zote Sio Sawa
Kiwango Cha pombe hupimwa kwa kiwango, au asilimia ya hii kemikali "ethanol" katika mchanganyiko wote kwa ujumla ndani ya chupa ya pombe. Ndani ya chupa ya Pombe, Hakuna pombe peke yake, au ethanol tu, Bali Kuna kiwango kikubwa Cha kemikali na virutubisho vingine. Mfano, kuna maji, madini, vizuia kuharibika, vizuia oksijeni, vitia ladha n.k. na hii ndiyo sababu, Kuna kipindi ambacho pombe huwa haiwezi kutumika zaidi, hii ni kwasababu nayo hutunzwa kwa sifa kama sifa za vinywaji vingine.
Kuna Aina mbalimbali za pombe. Hii inatokana na kilichotumika kutengeneza Pombe, vitia ladha vilivyowekwa, kiwango Cha Pombe iliyopo, aina ya pombe iliyopo, utengenezaji wake, na pia kutokana na matumizi yake. Utendaji wa pombe ndiyo sababu kubwa zaidi ya kupendwa kwake, na pia ndiyo sababu ya kukataliwa kwake.
Kuna migogoro mikubwa Sana juu ya utumiaji wa pombe. Na migogoro hii ipo katika kila ngazi. Mfano, Kuna migogoro kutokana na tofauti za mitazamo ya kiimani, mitazamo ya kiafya, mitazamo ya kiuchumi, na mitazamo ya kijamii na maadili. Migogoro hii haijaishia tu kutokana na tofauti za kiimani, Bali hata ndani ya Imani. Mfano, ndani ya wakristo wapo wanaoamini kuwa ni ruhusa kunywa pombe, na wengine hawaamini Kama imeruhusiwa. Na hata neno pombe katika Biblia limeonekana kutumika japo kwa lugha tofauti tofauti, lakini limetumika katika namna zote mbili, yaani kana kwamba yaweza kubalika au katiliwa.
Na hii ndiyo Sheria ya asili ya migogoro mikubwa yote, lazima iwe na pande mbili zenye hoja zinazokaribiana uzito. lakini pia, haipingiki katika Sheria za asili kuwa, huwa Kuna ukweli mmoja tu ijapokuwa unaweza kuwa na pande mbili, mfano; kuua ni Dhambi na Biblia umeandika Usiue, lakini upande wa pili huwezi kuishi bila kuua Mimea, Bakteria, wadudu, na Wanyama, na hata Mungu ataua Wadhambi Jehanamu. Na hiyo ndiyo sababu kubwa ya mpaka leo Sayansi bado inatafuta nadharia moja ya kuelezea ukweli wote bila kutofautisha, inaitwa " theory of everything" . Albert Einstein alikufa akiwa bado anahangaika kutafuta "unified theory of everything". Hivyo Basi, hata kwa pombe stori ni hii hii.
Kumbuka!
Si kweli kuwa kila kinachofahamika kuhusiana na Pombe ni madhara na hatari kiafya, sehemu ifuatayo tutaanza kuangalia hatari zaidi kisayansi, lakini mbeleni, tutaangalia hoja za muhimu pia kuhusiana na Pombe ijapokuwa si Kwa mantiki ya mtazamo unaweza fahamika na Kila mtu, au walevi wa zama hizi.
BIOLOJIA YA POMBE MWILINI
Pombe au alcohol katika mwili hupitia Aina mbalimbali za matendo ya kibiolojia "metabolism" , na haya huwa yakiendana na sehemu husika ambayo pombe hupita au fika. sehemu hii tutaangalia matokeo ya pombe katika kila sehemu ambapo huwa inapita.
POMBE MDOMONI
Unapokunywa Pombe ikifika katika mdomo, kwanza huanza kwa kukutana na seli za kuhisi za ulimi. Ladha ya pombe ni chungu ‘’Bitter’’, ijapokuwa watumiaji huamini kuwa pombe ina Ladha ya utamu kama sukari. mara nyingi hisia ya utamu wa sukari katika pombe huwa ni madhara aidha ya kijenetikia yanayotokea kutokana na unywaji sana uliopo, au uliokwisha pita, na pili utamu wa pombe mara nyingi huwa hausababishwi na kemikali pombe mdomoni, bali namna ubongo unavyoichakata pombe. sehemu za mbele kidogo tutaliangalia hili kiundani.
Mdomoni kiasi kidogo cha pombe hufyonzwa na tabaka la juu la seli za ulimi, na kuanza kuingia kwenye damu kwa kiwango kidogo.
POMBE TUMBONI
Baada ya Pombe kufika tumboni, miongoni mwa vitu ambavyo huwa vikitokea kwanza kabisa, kwanza, Tumbo huwa na kimeng’enya au enzyme zinazoitwa ‘’Alcohol dehydrogenase’’, hizi kazi yake kubwa huwa ni kuivunja ile pombe. Kumbuka, Pombe ina uwezo mkubwa sana wa kupenya katika ukuta wa tumbo na kuingia katika damu, na ina huu uwezo kwa kuwa molekuli za pombe ni ndogo sana na hazina chaji, kwa hiyo hazizuiliki kirahisi, na hivyo basi, ukishakunywa pombe tumbo lako huakikisha linawahi kuivunja hii pombe.
Na kitendo hiki huitwa ‘’first path mechanism of alcohol’’, Tumbo huongeza kujikunjakunja ‘’Gastric motility’’ ili kuifanya pombe isikae sana tumboni, hiki kitendo huitwa ‘’gastric emptying’’. Lengo kubwa ni kuwa, kama itakaa sana tumboni, hata kama itavunjwa vunjwa, bado itasababisha madhara makubwa sana kwa kuwa, kuna itakayo pita na kuingia kwenye damu na kusambaa katika mwili wote.
Pombe bila chakula
Mtu anayekunywa pombe huku hajala chakula, au hana chakula tumboni, huathirika zaidi kuliko yule aliye na chakula tumboni. Hii ni kwa kuwa, mwenye chakula tumboni hupunguza kiwango cha pombe kitakachokuwa kikipita kuingia kwenye damu, hii ni kama kusema, chakula huizuia pombe isipenye kirahisi.
Wale ambao huwa wakinywa pombe na kuchanganya na Limao, huchelewa kulewa kwa sababu ya tabia ya Limao, ambalo lina asidi ‘’carboxylic acid’’, kuungana na pombe au ‘’alcohol’’, na kuunda kemikali zinginezo kama ‘’esters’’. Hawa hupunguza kiwango cha pombe inayobakia huru kuingia katika damu, na kuelekea katika ubongo ambapo stori ya kulewa huanzia.
Kwanini Mungu aliweka AD tumboni kama hataki watu wanywe Pombe?
Kimeng’enya au enzyme ‘’alcohol dehydrogenase’’ huivunja pombe na kuunda molekuli kadhaa, Kuanzia na kemikali inayoitwa ‘’Acetaldehyde’’. Hii kemikali ambayo huundwa baada ya kumeng’enywa pombe ni Sumu kubwa sana kwa kufanya yafuatayo:
Husababisha Matatizo ya Kijenetikia, na hii ni kutokana na tabia yake ya kupenda Kwenda kuifungafunga DNA. Hii ‘’acetaldehyde’’ ni kikambakamba. Hiki huenda kwenye molekuli za muhimu kabisa za mwili, ikiwemo na vimeng’enyaji au enzymes, na kisha kuzifunga funga hata kuzifanya zishindwe kufanya kazi zake vizuri.
Pia husababisha Uharibifu mkubwa wa Tishu za mwili, Acetaldehyde ni kemikali ambayo mara nyingi sana, hupelekea kuzalishwa kwa kemikali sumu za mwili, tulizoziona kwa sehemu iliyopita, zinazoitwa ‘’Reactive oxygen species’’, hizi tuliona kazi zake kubwa zaidi ni kusababisha ‘’Oxidation’’, ambayo ni kama kuchubua chubua kila molekuli za muhimu kabisa za mwili, na pia, huusiana na kufanya matatizo makubwa sana ya mfumo wa fahamu, ijapokuwa tutaangalia zaidi huko mbele, ila unaweza tambua ni kwa namna gani, neva za mwili huwa zikichubuliwa chubuliwa, na kuleta matatizo katika utendaji wake.
Matatizo katika matendo ya kibiolojia, hebu tazama namna mwili wako umejawa na maelfu ya matendo ya kibiolojia, ambayo hayo yote yanahitaji utendaji wa ‘’enzymes’’, yanahitaji kutokuwepo kwa zile sumu kama ‘’Reactive oxygen species au ROS°’’. na pia, yanahitaji tishu na seli zilizo bora. Na sasa basi, uwepo tu wa acetaldehyde yenyewe, kwanza, huathiri utendaji wa enzymes zote, lakini pili, huzalisha hizo ‘’ ROS°’’, ambazo, huathiri utendaji mzima wa matendo ya kibiolojia. Na madhara yake ni mtu kuwa matatizo chungu mzima, ya mifumo mingine kama ya figo, ini n.k. hii ni kwa kuwa tayari mfumo wa mahesabu wa kemikali za mwili umeharibiwa.
Matatizo ya Moyo na Upumuaji kupita kiasi.
Hii ni kutokana na matatizo ya mfumo wa fahamu, unaokuwa umeathiriwa, tutaona hapo chini, madhara ya pombe kwa ubongo
Shida katika Mfumo wa Kinga
Mara nyingi kutokana na shida ya kuharibiwa kwa tishu, na sehemu mbali mbali za mwili, kutokana na acetaldehyde na ‘’reactive oxygen species’’. Ambazo, husababisha ‘’oxidative stress’’. Moja kwa moja, huishia katika kupelekea uvimbe katika sehemu mbalimbali za mwili ‘’inflammation’’, na madhara mengine.
Je wajua tofauti ya kuwahi kulewa?
Kiwango hiki cha enzyme ‘’alcoholdehydrogenase’’ kimetofautiana baina ya watu. Hii husababisha baadhi ya watu, kuweza kuvunja pombe haraka, na kwa ufanisi zaidi ya wenzao, kwa hiyo, utakuta mmoja akiwa na uvumilivu wa pombe zaidi ya mwenzake, au akiwa haoneshi kudhurika na pombe kuliko mwenzake.
Tofauti hizi huanzia pia kutokana na mabadiliko katika jenetikia, mfano huaminika watu wa mashariki ya Asia, wanakiwango kikubwa cha ‘’Gene’’ inayoitwa ‘’ALDH22’’ ambayo huwa ikishusha utendaji wa ‘’alcohol dehydrogenase’’. hii huwafanya kuwa wahanga wakubwa zaidi wa pombe.
POMBE KATIKA INI
Hii ni sehemu ambayo hushughulika zaidi na Pombe, katika namna ya kupambana nayo.
sayansi ya Ini dhidi ya Pombe
Ini huwa na mtindo wa kushughulika na vitu au kemikali za kigeni kama dawa. Na huwa na sehemu mbili za kuzishughulikia kemikali hizi ngeni, yaani ‘’Phase I na Phase II’’. kwa phase I ini huzifanya kemikali ziwe na chaji ili izishughulikie vizuri. Huzipa chaji kupitia aidha (oxidation,reduction, hydrolysis, hydration..) haya matendo yote yanamaanisha tu kuwa, ini kwa kutumia kemikali zake zilizopo unapokula chakula, huongeza chaji kwa kemikali ngeni kulingana na aina yake. Mfano, inaweza zifanya ziwe na chaji Chanya ‘’oxidation’’, au ziwe na hasi ‘’reduction’’, au kuziondoa maji ‘’hydrolysis’’, au kuziongezea maji ‘’hydration’’.
Zikishakuwa na chaji au ‘’polar’’, ini huzishikamanisha na kemikali zake kama (vitamini B2, B3, B6, na B12, Folic acid, Flavonoids na Glutathione), na sasa basi, zikishashikiliwa na kemikali hizi ngeni, hii Ndiyo huwa hatua ya ‘’Phase II’’. ambako huko, Ini kwa kutumia kemikali au ‘’chembechembe hizi, sumu hutolewa nje ya mwili kwa njia ya mkojo, au nyinginezo. Haya matendo huitwa ‘’Conjugation pathways’’. Na hapa kuna matendo kadhaa kwa mfano kuna (Glucoronidation, acetylation, Glutathione conjugation, amino acid conjuagation, methylation, n.k).
Hapa Hapana changamoto yoyote, ukisikia mfano ‘’Glucoronidation’’, maana yake ni kuwa, ini limeongeza kemikali inayoitwa ‘’UGT’’ au kirefu ‘’UDP-Glucoronosytransferase’’ kwa yule kemikali mgeni aliye na chaji. huyu UGT humshikilia kemikali Sumu mpaka atakapomtoa kupitia aidha mkojo, Nyongo, au Kinyesi. Na hii ndiyo namna sumu hutolewa nje ya mwili. Kwa hao wengine pia huwa ni hivyo hivyo, mfano ukisikia ‘’Acetylation’’ maana yake saivi mdakaji ni ‘’acetyl.’’, ukisikia ‘’Glutathione conjugation’’ maana yake mdakaji ni ‘’Glutathione.’’, ukisikia ‘’Amino acid conjugation’’ maana yake mdakaji ni ‘’amino acid.’’. na ini huweza kufanya hii kazi kwa msaada wa kemikali zake ikiwemo (Methionine, Cysteine, Magnesium, Glutathione, Vitamini B5, B12, C, Glycine, Taurine, Glutamine, Folic acid na Choline)
POMBE NA INI
Kwanza utangulizi Pombe huwa haipiti katika njia za ini za kujilinda. Kwa hiyo hayo maelezo ya juu hutumika kwa sumu na dawa zingine ila sio kwa pombe. Pombe huwa na njia zake maalumu. ambazo ini hushughulika nazo. Zipo njia kuu tatu za pombe kuchakatwa katika ini.
Kupitia Mchakataji au Enzyme ‘’Alcohol dehydrogenase’’ au ADH
Kumbuka huyu bwana tumboni yupo kwa kiwango kidogo sana ukilinganisha na kiwango chake katika ini. Na huyu ndiyo mvunjaji mkubwa zaidi wa pombe katika mwili. Yeye hubadilisha Pombe, au alcohol, na kuunda ile sumu niliyoisema inaitwa ‘’Acetaldehyde’’. Tumeshaona madhara ya acetaldehyde katika mwili, lakini pia, badiliko hili huusisha badiliko la kemikali zinazoitwa ‘’nucleotides’’ kubadilika kutoka katika NAD⁺ na kuunda NADH.
Pia acetaldehyde ambazo huwa zikiundwa, kwa kuwa ni sumu, huvunjwa zaidi haraka sana kupitia enzyme mwingine anayeitwa ‘’aldehyde dehydrogenase’’, ambaye huyu huivunja acetaldehyde ili kuunda kemikali yenye madhara kidogo, inayoitwa ‘’acetate’’ . na hii kemikali ‘’acetate’’ hubadilishwa zaidi ili kuunda ‘’acetyl CoA’’. Ambayo huingia katika hatua ya pili ya kuzalisha nishati, hushilikishwa katika uundaji wa mafuta ‘’lipogenesis’’, na nyingine hutolewa.
Kitambi Cha Pombe
Miongoni mwa madhara makubwa sana ya pombe kuchochea kushamiri sana Kwa NADH ni kuwa, huenda kuathiri balansi ya matendo ya nishati katika hatua ya pili ya uzalishaji nishati ya mwili inayoitwa ‘’Kreb’s Cycle’’. Na hii ni kutokana na kuwa, hatua hii hulenga kuzalisha kiwango kikubwa cha ‘’NADH’’. lakini mwili ni kama huona tayari kuna ‘’NADH’’ za kutosha. Hizi ‘’NADH’’ huelekea katika hatua ya tatu ya uzalishaji wa nishati inayoitwa ‘’ETC’’ au ‘’Electron transport chain’’, na huko husababisha kiwango kikubwa sana cha nishati au ‘’ATP’’. Na kiwango hiki cha nishati, au ‘’ATP’’ husababisha kupungua kwa uzalishaji zaidi wa NADH katika hatua ya pili ‘’kreb’s cycle au Tricarboxylic acid cycle’’ kwani tayari kuna nishati ya kutosha.
Madhara yake hasa huwa ni Kiwango kikubwa cha kemikali inayoitwa ‘’Acetyl coA’’ kubakia huru. na kemikali hii huishia kupelekwa katika ujenzi wa Mafuta, ambapo huko, hii kemikali huwa kama vile tofali lilivyo la msingi kwa ujenzi wa nyumba. Kwa hiyo mtumiaji wa Pombe lazima atajikuta akiwa na kakitambi.
Pia kuvunjwa kwa acetaldehyde kwa kutumia enzyme anayeitwa ‘’aldehyde dehydrogenase’’ hupelekea kuzalishwa sana kwa kemikali ‘’Acetate’’, na hii kemikali hatma yake kubwa huwa ni kubadilishwa ili iwe ‘’acetyl coA’’. na Kwa kuwa tumeshaona kuwa ‘’acetyl coA’’ haiwezi kutumika kuzalisha zaidi nishati, kwa hiyo hamna namna yote huishia kuunda mafuta. Masomo mbalimbali yanaonesha kuwa matendo haya yanapotokea huambatana pia na kusisimuliwa sana kwa enzymes za uundaji wa mafuta ‘’de novo-lipogenesis’’. Kwa hiyo ukichanganya haya yote, unaweza pata sababu kwanini walevi wengi huishia kupata vitambi.
Kupitia vivunjaji ‘’microsomes’’ CYP2E1
Njia hii japokuwa haichakati kiwango kikubwa sana cha Pombe kama ile iliyopita. Lakini nayo huvunja kiwango kikubwa cha pombe, au alcohol, na kuunda kemikali ileile sumu tuliyoiona inaitwa ‘’Acetaldehyde’’. Na baada ya kuundwa kemikali hii, hatua zote hujirudia zile zile kama za juu.
Wanawake na kulewa haraka
Swali hili tunaweza kulijibu kiufupi kwa kuangalia kiwango cha maji mwilini. Wanaume wana kiwango kikubwa sana cha maji mwilini ukilinganisha na wanawake. kiwango hiki cha maji hupelekea pombe nyingi kuyeyushwa ndani ya maji na hivyo kuchelewesha au kupunguza kiwango cha pombe inayoingia mara moja kwenye damu kama ilivyo kwa mwanamke.
Hii ni sababu ya wanawake kulewa haraka zaidi ya wanaume. Lakini pia masomo kadhaa huonesha, hata kiwango cha vimeng’enyaji au enzymes za kuchakata pombe zipo kwa wingi zaidi kwa wanaume ukilinganisha na kwa wanawake. Mabadiliko ya kihomoni ya miezi kwa wanawake, huathiri zaidi uchakatwaji wa pombe mwilini, na hii hujaribu kuonesha madhara zaidi ya pombe kwa mwanamke.
Kuchakata Pombe kupitia ‘’Catalase’’
Huyu ni enzyme ambaye ana tabia ya kuvunja kemikali inayoitwa ‘’Hydrogen peroxide’’ . kemikali hii huzalishwa katika miongoni mwa matendo ya kuchakata pombe. Na kwa mantiki hiyo huyu bwana huwa hausiki moja kwa moja ila ana mchango mkubwa sana.
MADHARA YA POMBE KATIKA UBONGO
Hapa ndipo penye Subira zaidi ya wasomaji. Kwanza kabla ya yote ni muhimu kutambua baadhi ya vitu, au sifa za msingi za seli katika Ubongo. Kwa kuwa hizi ndizo hushambuliwa hata mtu mmoja asemwe kuwa ‘’amelewa’’, au aitwe ‘’mlevi’’. Seli ya ubongo au ‘’Neuron’’ huwa ikisisimka kama ndani kutakuwa na chaji Chanya (+ve). Lakini pia seli ya ubongo huwa na msisimko mdogo sana kama ndani kukiwa na chaji Hasi (-ve). Mabadiliko ya ndani kuwa na chaji hasi zaidi, au kuwa na chaji Chanya zaidi, huwa yakitawaliwa au kuongozwa na uwepo wa chembechembe maalumu kabisa nje ya seli zinazoitwa ‘’neurotransmitters’.
Hizi kazi zake huwa ni kuruhusu chaji Fulani zipite zaidi, au zitoke, au zisiingie kabisa, ili seli za ubongo aidha zisisimke, au zisisisimke kabisa. Na kemikali hizi huwa hazifanyi kazi tu zenyewe, huwa na utaalamu wa kusoma hali mbali mbali za mwili, kupitia kemikali kadha wa kadha zinazopita katika ubongo, na kuamua nini kinapaswa kuamshwa, na nini kinapaswa kulazwa. Pia mageti haya huwa yakitawaliwa na connections mbalimbali, kutoka sehemu za ubongo. na ndiyo maana, unaweza kuamua na ukasisimka. lakini pia, unaweza usiamue, lakini kuna vitu vikakusisimsha tu. Hii ni sawa na kusema, mageti haya, hufanya kazi kulingana na vitu kama ‘’codes’’. ambazo hizo, zikifika tu kwenye sensa zake, au receptors zake, basi huyafungua.
Pombe huyafungua na kufunga mageti haya, kulingana na aina zake. Pombe huwa haifungui kila geti, lakini katika ubongo, Pombe hushughulika na miongoni mwa mageti muhimu sana, na hapa tutayaona na tabia na madhara yake. Kumbuka kuwa, kemikali hii ya pombe inayosababisha zaidi madhara katika haya mageti, inaitwa ‘’Acetaldehyde’’. Ambayo, ndiyo sumu tuliyokwisha iona kwa sehemu za juu.
GETI LA GABA ‘’GAMMA AMINO-BUTYRIC ACID’’
Geti hili sifa yake kubwa huwa ni ‘’KUZUIA’’ au pia huitwa ‘’’major inhibitory neurotransmitters’’.
Katika picha juu, hivyo ndivyo mfano mdogo wa circuit ya geti la GABA linavyoonekana. GABA huwa na sifa kuu ya kuruhusu Potassium itoke nje, na Chloride iingie ndani. Na kufanya ndani kuwe na chaji hasi zaidi. Kitendo hiki ambacho pia huitwa ‘’hyperpolarization’’ huifanya ‘’neurons’’ ipoe, au isisimke sana. Kama unavyoona katika huo mchoro. kuna maneno mawili ‘’Phasic inhibition’’. hiyo hutokea zaidi kipindi cha kuzuia hali Fulani, lakini kwa hiyo ‘’tonic inhibition’’, hiyo huwa ikitokea zaidi kipindi cha kawaida katika ubongo.
POMBE IKIFIKA KWENYE GABA
Kama unavyoona hapa, pombe huchochea kabisa kazi ya ‘’GABA’’ na kupelekea mgandamizo mkubwa zaidi wa seli za ubongo.
Mtu anayekunywa pombe anachochea kujizima mwenyewe, hebu tuangalie nini ni matokeo makubwa zaidi ya kitendo hiki cha kuchochea kazi ya GABA.
MATOKEO YA KIAKILI YA KUNYWA POMBE KATIKA GABA
KUONDOA MAWAZO AU STRESS/ KUJISIKIA AMANI
Kama unavyosikia nyimbo nyingi wakisema, bora tunywe pombe kuondoa Mawazo. Ni kweli wapo sahihi, kwa kuwa, kiwango kikubwa zaidi cha ‘’neurotransimitters’’ za GABA, kipo katika sehemu za ubongo wa mbele ‘’prefrontal cortex’’, zipo katika ubongo wa kumbukumbu ‘’hippocampus’’, na pia zipo katika ubongo unaotawala nguvu katika miondoko ‘’basal ganglia’’.
Ukiangalia mlevi kwanza, hawezi kuwaza. kwa kuwa, kiwango kikubwa cha GABA kilichopo katika Ubongo wake wa mbele, ‘’prefrontal cortex’’, huzuia kabisa shughuli za kufikiria. na hii humsababisha mtu huyu, asiwe na msongo wa Mawazo.
Pia kiwango kikubwa cha GABA kilichopo katika maeneo yanayohusiana na kumbukumbu, humfanya mtu huyu asiwe na uwezo wa kuunda kumbukumbu. na kukumbuka taarifa za matendo yaliyopita, kwa muda mrefu kidogo nyuma. Na hii humsahaulisha stress alizokuwa nazo. Na ndiyo maana, utakuta wasanii wengi wakiisifia pombe.
KUWA DHAIFU WA MIONDOKO KAMA KUTUMIA MISULI
Pombe kwa kawaida kama tulivyokwisha iona huwa ikizalisha GABA. ambazo tumeona kuwa zimejaa sana katika maeneo ya Ubongo yanayoitwa Basal Ganglia. sehemu hii hutawala matumizi ya nguvu katika misuli. Kwenye basal ganglia kuna nyuklia moja ambayo huitwa Substantia Nigra yenye eneo linaloitwa ‘’Pars Compacta’’. Huko kumetapakaa GABA. Matumizi ya Pombe huchochea GABA na kuathiri kabisa uwezo wa kutembea na kufanya shughuli nyingine za kutumia misuli.
Walevi wengi huwa wanapata shida kuzungumza vizuri, pia wanashindwa hata kujisaidia vizuri, ni rahisi sana kwa mlevi kujisaidia haja ndogo, na hata kubwa. Mlevi hata kufungua jicho kwake huwa ni shughuli kubwa sana. Ukitaka kumkamata mlevi vizuri, wewe mchoree mstari halafu umwambie aufuate, au asimame kwa mguu mmoja. Shughuli hizi zote kwa Pamoja huitaji maeneo mengi ya ubongo ‘’higher cerebral functions’’ ambapo kwa mlevi hawezi kwa kuwa sehemu nyingi amekwisha zigandamiza.
HUPUNGUZA HISIA ZA TAARIFA KUTOKA MILANGO YA FAHAMU
Mtu aliyelewa kama ambavyo tuliona kuwa hata uwezo wake wa kufikiria ni hafifu. Pia huwa na tabia ya kupuuzia moja kwa moja taarifa anazoziona. Na ndiyo maana, ajali nyingi za barabarani hutokana na ulevi. Hii ni kwa kuwa, ubongo wake ameshauzuia kuweza kufanya kazi ya kufikiria na kufanya maamuzi sahihi.
HUSEMA UKWELI
Kwa kawaida sifa kubwa sana ya ubongo wa mbele ni kuchanganua madhara na faida ya kila maamuzi. Na kazi hii huufanya uwe na sifa kubwa sana ya kugandamiza taarifa nyingi sana ambazo huwa umeziona kuwa zina hasara nyingi zaidi ya faida. Hebu chukulia mfano wa taarifa hizi: mtu mmoja amemtamani mke wa Jirani yake, ila hujizuia kwa kuwa Jirani yake ni rafiki yake, au yeye amekwisha kuoa. kama mtu aliyelewa amebeba siri ya udhaifu wa mwenzake, ambapo siku zote hujizuia asiseme. Mtu huyu anapolewa, taarifa hizi ambazo zilikuwa zipo katika makundi yaliyozuiliwa sana, kwa msaada wa GABA, sasa huwa hatarini sana kuzungumzwa.
GETI LA GLUTAMATE/NMDA ‘’N-Methyl D-Aspartate’’ RECEPTOR
Hii ni neurotransmitter ambayo ina sifa kuu ya kuwa na matokeo ya kusisimua. Pia huitwa ‘’stimulatory neurotransmitters’’. Hii inapomsisimua mtu, humfanya ajisikie raha sana. Sasa pombe ndiyo msisimuaji mkubwa sana wa hizi kemikali za ubongo. Pombe yenyewe huwa haizisisimui, huwa unazigandamiza zaidi ila matokeo yake ni kuzisimua zaidi.
Kutoka katika hii picha, kuna baadhi ya vitu vya msingi ya kuvizingatia. Ila mfano mwepesi zaidi wa kuielewa ni kwa namna hii, chukulia mfano ukute mnyama ameingia katika mfuko. Halafu hebu funga huo mfuko kwa ghafla uone! yule mnyama atakuwa akikurupuka sana kwa kutaka kutoka hata atakapo choka kabisa. Hivyohivyo hapa Pombe inapofika kwa haya mageti husababisha chaji nyingi Chanya ziingie, na kisha pombe ikishajishikilia katika mageti haya, huzuia geti hili lisiruhusu zaidi vitu kuingia, au Calcium kuingia. Kwa hiyo, awali ililifanya liwe na Chanya sana, na mlevi akafurahi sana. Lakini baadae geti hili likawa halina uwezo wa kufanya kazi kabisa. Na tatizo hili hupelekea matatizo yafuatayo ya ubongo
MATOKEO YA KIAKILI YA KUCHEZA NA GETI LA NMDA
KUJISIKIA HISIA ZA FURAHA SANA NA MSISIMKO ‘’euphoria’’
Watu wengi wanapokunywa pombe huwa na hisia za furaha sana. Na ndiyo maana kama wapo kwenye maeneo yenye muziki, utawakuta wakiamka na kuanza kucheza. Hisia hizi za msisimko mkubwa sana, na hisia za kuamsha amsha, ni matokeo ya kile tulichokiona katika sehemu ya juu, namna ambavyo mageti haya ya NMDA yanavyokuwa yakisisimka. lakini baada ya muda pia utendaji wake huanza kushuka.
Mtu aliyelewa ni rahisi sana kuzungumza kwa sauti, au kupiga kelele kwa sauti. Na pia ni rahisi sana kujihisi ana uwezo mkubwa sana, na ndiyo maana walevi wengi sana huwa na mikwara ya kuwatishia wenzao. Tabia hizi zote huusiana na matokeo ya neurotransmitters za Glutamate. Pamoja na matokeo ya GABA.
KUCHANGANYIKIWA ‘’drowsiness’’, KUPOTEZA FAHAMU ‘’blackout’’ & KUSHINDWA KUHEMA ‘’respiratory failure’’.
Mara nyingi kadri muda unavyozidi Kwenda na mtu amekunywa kiasi kikubwa sana cha pombe, basi dalili zake huzidi kuwa mbaya. Hii huanzia kwanza mtu anapokuwa anajihisi hayupo sawa, akihisi kuchanganyikiwa, mfano mtu huzungumza hata maneno yasiyofahamika. Haya yote huwa ni matokeo ya kupungukiwa msisimko, na kuongezwa kwa mgandamizo katika sehemu nyingi za ubongo.
Lakini hufika wakati ambapo, mtu hupoteza fahamu. Katika hatua hii, hata ule uwezo kidogo wa utambuzi nao hupotea kabisa. Hiki ni kiwango ambacho kuna kiwango kikubwa sana cha madhara ya sumu za pombe. Kuanzia hizi hatua, hali ya ubongo huwa ni mbaya sana, kwa kuwa, sasa ubongo huanza kushindwa kutimiza majukumu yake, kutokana na mgandamizo mkubwa sana dhidi ya kazi zake. Na hili huweza hata kupelekea matatizo makubwa zaidi ya utendaji wa mwili, ambao hutegemea mwongozo kutoka kwa ubongo.
Kushindwa kuhema ambako huweza kupelekea kufa, huku huwa kutokana na mgandamizo mkubwa sana katika sehemu za ubongo ambazo hutawala matendo yasiyo hiari kama kuhema. Mara nyingi huwa ni sehemu za Medulla oblangata na sehemu zingine za ubongo.
MADHARA YA URAIBU ‘’withdrawal effects’’
Unapotumia sana pombe, kwa kuwa huwa ukikandamiza sana utendaji wa Glutamate, na kuchochea sana GABA. Basi Ubongo hutengeneza mazingira ya kujikinga na matatizo hayo. Na hapo ndiyo mwanzo wa Ubongo kupunguza kiwango cha ‘’Receptors’’. ili kama utakunywa, basi usisababishe madhara makubwa sana. Hii humsababisha mlevi atakapokunywa chupa zilezile, ahisi bado hazijatosha. Hali hii humfanya mlevi aendelee kunywa na kunywa zaidi kila siku, na ubongo hupunguza zaidi na zaidi kila siku.
Ikitokea siku mtu huyu akaacha, basi hujikuta ana kiwango kidogo sana cha GABA na GLUTAMATE ambazo zimebakia kufanya kazi za kawaida. Na hivyo huwa akijisikia hali mbaya sana. Ambayo humtesa sana kiakili. Na huwa na Msongo na mateso makubwa sana.
POMBE HUCHOCHEA UZALISHAJI WA HOMONI DOPAMINE NA SEROTONIN
Hizi ndizo homoni humfanya mlevi ajisikie raha sana. Kama mlevi akiona pombe anachanganyikiwa kabisa, basi ujue hiyo ndiyo Dopamine. Na kama ukimwona mlevi akianza kunywa pombe ana furaha sana hata anahisi pombe ni tamu sana, basi ujue ni serotonin.
Kwa mara ya kwanza mwaka 2018 october 2022, Mark Brodie ambae ni Professor wa Fiziolojia na Biofizikia katika chuo cha UIC cha Udaktari, aligundua kuwa, Pamoja na kufahamika kuwa mtu akinywa pombe husababisha Ubongo wake ndani katika sehemu moja inayoitwa ‘’VTA’’ au ‘’ventral tegmental area’’ kuzalisha homoni ya Dopamine. huyu bwana aligundua mpaka sehemu husika kabisa inayohusika. Aligundua kuwa Pombe huenda kublock chaneli ya Potassium inayoitwa KCNK3. Ambayo chaneli hii ipo ndani ya ukuta wa seli za ubongo katika sehemu hiyo ya VTA.
Unapokunywa pombe huwa inaenda katika sehemu ya ubongo maeneo ya shina la kati kwa chini kwenye sehemu inayoitwa ‘’VTA’’ au ventral tegmental area. Na sasa basi, ikishafika pale huichochea sana neuron ya GABA, na kuifanye isizalishe kabisa neurotransmitters GABA, ambazo zingeenda kuizuia neuron ya pili ya dopamine . Swala hili huifanya neuron inayozalisha Dopamine kuzizalisha nyingi sana katika sehemu ya Ubongo inayoitwa ‘’Nucleus accumbens’’, eneo hili lipo maeneo ya ndani ikizungukwa na maeneo ya hisia ‘’limbic system’’. Na swala hili humfanya mtu ajisikie raha sana kwa kuwa kiwango kikubwa sana cha dopamine kimezalishwa.
Sehemu hii inahusisha majibu Kwa mtazamo wa Dr Shoo#
MASWALI YAULIZWAYO ZAIDI?
Je ni Dhambi kunywa Pombe?
Kama unayosababu ya kunywa pombe unaweza kujitetea. Wanaokunywa Paracetamol pia hunywa Pombe. Wanaotumia Dawa za Maumivu na za Nusu kaputi nao hutumia pombe. Pombe huwa ni msaada Kwa wanaopitia Hali ngumu za Msongo wa mawazo, zikiwa kama Dawa, au "Anti-depressants".
Mithali 31:
6 Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini.
Give strong drink unto him that is ready to perish, and wine unto those that be of heavy hearts.c
Give strong drink [as medicine] to him who is ready to pass away, and wine to him in bitter distress of heart.
Unywaji Kwa maelezo ya juu hauambatani na madhara makubwa yaliyoelezwa Kwa sehemu iliyopita, ila unasaidia kuondoa madhara makubwa zaidi yanayotokana na hali anazozipitia mnywaji.
Kama Mungu hakutaka watu wanywe Pombe, kwanini aliweka AD tumboni?
Kuweka kivunja Pombe "Alcohol dehydrogenase" tumboni ni ishara kuwa Mungu alishajua Mwanadamu atakuwa mnywaji wa pombe, na hasa kupitia Vyakula ambavyo huwa vikivunda na kuzalisha pombe "ethanol" tumboni.
Kwanini Mababa wa Imani kama Nuhu, Lutu, n.k. Walikunywa Pombe?
Wengi wao Walikunywa katika mantiki ya Juisi za zabibu, ambazo zilikuwa na kiwango kidogo pia Cha Ethanol ambayo ingeweza kulewesha, lakini kabla ya kujibu swali hili, ni muhimu kujiuliza maswali makubwa zaidi yafuatayo.
Je, Pombe ni kileo, au Mchanganyiko wa Juisi yenye kileo?
Kwa asili enzi za zamani za Biblia, na hata Afrika, Pombe zilikuwa ni Juisi zenye vileo kidogo. Kwa Sasa , pombe ni Vileo vyenye asilimia mbalimbali zinazotunzwa katika kemikali kama Juisi, zikifanywa kuvutia Kwa kuongezewa Ladha za kisasa.
Kwa zamani, mfano mzuri za Yesu katika harusi ya Kana, Divai ilikuwa ni Juisi ya zabibu ambayo hata Sasa inashauriwa Kwa kuwa na virutubisho hasa Antioxidants za Reservatrol, na Polyphenols mbalimbali ambazo ni virutubisho vilivyokwepo katika maganda yake.
Asilimia ya ethanol au pombe ilikuwa ni ndogo sana kiasi kwamba ingemuhitaji mtu kuwa Mlevi wa makusudi Kwa unywaji uliopotiliza. Mfanano mzuri kivirutubisho ni Mbege Kwa wachaga, au Ulanzi Kwa Wahehe, Pombe ya mnazi Kwa watu wa pwani, au Umqomboth Kwa Wazuru. Unywaji uliambatana na namna za kujisaidia kimawazo, lakini madhara yake yalipunguzwa Kwa faida pia zilizokuwepo, pia kwa kiasi kidogo cha ethanol iliyokuwepo. Madhara yalikuwepo hasa Kwa Walevi waliokubuhu Kwa kukosa kiasi, au uraibu.
Je unywaji wa Pombe unaweza shauriwa kiafya?
Marazote wasio wanywaji wa pombe huwa Bora zaidi ya wanywaji kiafya. Kipindi tafiti zinapoonyesha kuwa unywaji wa Redwine unafaida kiafya, basi ulaji wa matunda ya zabibu Moja Kwa Moja una faida zaidi.
Kipindi tafiti zinaonyesha unywaji wa Redwine kidogo unachochea hisia za Mapenzi "Libido", utafiti unaonyesha kiwango kidogo hichohicho Cha Ethanol kinapunguza uwezo wa kufanya mapenzi.
Lakini katika mantiki Pana zaidi, unywaji wa Pombe unaweza kuwa wa muhimu katika maisha ya baadhi ya watu, na hasa; watu waliokatika mazingira ya stress za mara Kwa mara kama jeshini, na maisha ya kufanania. Hoja ya msingi ni kuwa; Kwa watu Hawa ambao maisha yao yapo katika stress za kudumu, ni vyema kuchagua aina za unywaji ambao hautakuwa na madhara makubwa, na hatari kubwa ya Uraibu. mfano mzuri ni kupitia swali lifuatalo?
Kwanini Unywaji wa Beer ni hatari zaidi ya Redwine, ilihali Beer in 4% na Redwine 12%?
Sababu ni kuwa, wanywaji wa Beer kutokana na asilimia yake ndogo ya alcohol, huweza kuinywa Kwa wingi sana, na hii huwapelekea kuathirika zaidi Kwa kujijaza kemikali Sumu nyingi sana. Na baada ya kipindi kirefu Cha unywaji huwa na kiasi kikubwa zaidi Cha alcohol kuliko hata wanywaji wa Redwine, ambayo nyingi yake huwa ina faida kadhaa za uwepo wa kemikali za maganda ya zabibu.
Hata hivyo, Kwa kadri usasa unavyozidi kuongezeka, hakuna Pombe ambayo Sio matokeo ya uchakataji wa kisasa ambao hupelekea kushamiri Kwa kemikali Sumu za kuitunza. Pombe nyingi huwa na pure ethanol ambayo huwa na matokeo ya Moja Kwa Moja katika Ubongo, na hii Ndiyo sababu; hakuna sababu ya kunywa pombe kiafya kama hakuna shida kiafya.
Kwanini Watu wanakunywa sana Pombe zama hizi?
Sababu kubwa ya unywaji wa Pombe, hata ulevi zama hizi, Sio sababu za kiafya. Wengi wa wanywaji huanza sababu ya mazingira yao; ukienda sehemu kama Kilimanjaro na Arusha, kunywa Pombe, na hata Kuvuta Bangi inaweza kuwa rahisi sana, si kwasababu ya kupenda, au kiafya, bali mazoea yaliyojenga tamaduni na hata makundi rika.
Ugumu wa Maisha, kuiga mitindo ya kisanii, na hisia za ujasiri na kutowaza baada ya kunywa, hutengeneza ujasiri wa kukabiliana na hisia za kukataa pombe, na kujipa motisha ya unywaji.
Je unaweza mhukumu mnywaji wa Pombe Kwa maamuzi yake?
Ni ngumu sana kumhukumu mnywaji kuliko ilivyo rahisi kumhukumu mzinzi. Kwa Mtu aliyeishi na walevi wengi, anaelewa Pombe zimebeba mengi sana katika maisha ya watu. Wengine hata wakitamani kuacha pombe, miili yao haiwezi Tena kustahimili maisha bila pombe.
Lakini kitaalamu, Kila mnywaji wa Pombe ana haki ya kubeba matokeo ya unywaji wake. Changamoto zote za Uzeeni, kuwahi kusahau, kuishiwa Nguvu za kiume, gauti, shida za uzazi, kushindwa kuona vizuri, Kisukari, kupungukiwa usikivu, ajali za barabarani, shida za kijamii, upungufu wa vitamin hasa B1 unaopelekea shida za Ubongo, shida za Uchumi, na matatizo yote ya kufanania hayapaswi kubebwa na mwingine zaidi ya mnywaji husika.
Je ni utajiri, Umasikini, au Makundi ndiyo Msukumo mkubwa zaidi wa Ulevi?
.....acha comment yako tujifunze zaidi.
Mwandishi na Mwenyekiti
Mtaalamu wa sayansi ya wanyama, mwanabiofizikia, na mwandishi wa vitabu vya kisayansi. Mwanzilishi wa Injili ya Sayansi — taasisi inayounganisha maarifa ya kisayansi na imani.
Shiriki makala hii
15 min
128 min