Inapakia...
Inapakia...

Dr Brighton Shoo
Mwandishi na Mwenyekiti
“Uchawi, Uganga Na Ushirikina 03/4 Utangulizi Sehemu hii inapaswa kusomwa kwa umakini sana. Awali inahusisha uchambuzi wa Imani za ushirikina au uchawi katika mtazamo wa elimu za kijamii zaidi ‘’Sociol…”
Uchawi, Uganga Na Ushirikina
03/4
Sehemu hii inapaswa kusomwa kwa umakini sana. Awali inahusisha uchambuzi wa Imani za ushirikina au uchawi katika mtazamo wa elimu za kijamii zaidi ‘’Sociology’’. Namna ambavyo mchawi au mtu yeyote ambaye anatumia sanaa za mtindo huu, anavyotambulika na misingi mikuu ya tabia zake. Inashangaza wengi hawajui kuwa Uchawi na Imani zote za kuufanania, ni kama Mti ambao una maelfu ya matawi na vijimatawi vidogo, na wachawi ni majani tu. Kuna aina mbalimbali za uchawi, na aina hizi wala hazina mtindo mmoja, na ndiyo maana haishangazi kuona, waganga wakishindana na wachawi, au wachawi wa eneo moja wakishindana na wengine, au hata kushirikiana. Uchawi ni mpana sana na hauna mfumo maalumu wa uongozi. Katika sehemu hii tutaangalia Misingi tu ya muhimu ambayo sanaa zote za uchawi, huwa nayo na kuizingatia. Baada ya kujua misingi hii, mtu yeyote aidha mchawi au asiye mchawi, anaweza sasa kuja kuelewa sehemu itakayofuata, ambayo tutaangalia kiundani sayansi zilizo nyuma ya sanaa hizi, na kwanini kadri siku zinavyosonga, zinazidi kuteka maelfu ya watu.
Historia Na Asili Ya Uchawi
Mwasisi mkubwa wa elimu za kuuchunguza Uchawi na mtaalamu wa saikolojia na jamii, J.G. Frazer Pamoja na mtaalamu mwingine wa saikolojia, W. Lehmann, katika toleo la pili la kitabu chao kilichoitwa ‘’Golden Bough’’ waliuita Uchawi kama ‘’ Elimu ya Kabla ya Sayansi’’ au ‘’Pre-science’’. Lehman aliwahi fanya tafiti za kina zaidi za Maisha ya wachawi, hasa katika mazingira ambayo huwa wakizungumza na yaitwayo ‘’Mapepo’’ , au Spirits. Na hitimisho la utafiti wake siyo ajenda kwa sehemu hii ya awali. Waasisi hawa wawili ambao kazi zao Pamoja na kukosolewa kwa baadhi ya taarifa au ‘’Data’’, wataendelea kukumbukwa kwa mchango wao mkubwa hasa katika kugundua miongoni mwa Sheria kuu za misingi ya utendaji wa uchawi ‘’Laws of Magic’’, ambazo tutaziangalia zaidi mbeleni. Kwa mtazamo wao na wa baadhi ya wengi wa wanasosholojia ‘’socialogists’’ wa awali ni kuwa, hapo zamani sana za maendeleo ya Binadamu, Binadamu alikuwa na imani kubwa sana ya mtindo wa kichawi au ‘’magic’’. hizi zinajumuisha Imani zote za kutenda vitu katika namna ya kutumia nguvu za kimiujiza, mfano, binadamu alitamani sana kutawala mazingira yake, kwa kutumia Mawazo yake, kunyakua vitu kwa kuvitazama, kubadilisha vitu kwa kuvitazama na kuvinenea n.k. lakini kadri siku zilivyozidi kusonga mbele, na akili yake ikazidi kuongezeka kimaarifa, ndipo alipogundua kuwa, binadamu binafsi hawezi kuitawala asili yake.
Mtazamo huu mpya wa kuwa binadamu hawezi itawala asili yake kwa Mawazo yake, ulichochea kuzaliwa kwa namna nyingine mpya ya mtazamo wa kijamii, ambao uliitwa ‘’Dini’’ au ‘’Religion’’. Kwa hiyo baadhi ya hawa wanasosholojia huamini kuwa, Imani za uchawi ndizo zilizotawala jamii ya watu wote huko awali, Kwa hiyo ni sawa na kusema ‘’Hapo zamani za kale, binadamu wote walikuwa wachawi, na baadaye, wakagundua uchawi hauna nguvu ya kutawala asili kupitia Mawazo, na hapo ndipo ikazaliwa Dini, dini ikasema kuna ‘’mungu’’ au ‘’god’’ ambaye ndiye anaweza kuitawala asili. Historia haishii hapo, binadamu akaendelea kuishi akiamini kuwa ‘’mungu’’ ndiye mwenye uwezo wa kutawala asili. Lakini ukafika wakati akili yake ikakua zaidi, na hapo akagundua kuwa, yeye ndiye aliyemtengeneza mungu, na hakuna mungu wa kutawala asili, asili inajiendesha yenyewe na anapaswa kuisoma asili kama mungu na sio mungu kuongoza asili, na hapo jamii ikaja na mtazamo mpya tena wa Sayansi. Sayansi iliazaliwa kwa kufeli kwa dini.
watu hawa hawakuishia hapa, bado imani nyingi zaidi za asili ya maendeleo ya sayansi, huonekana kutoka kwa Imani za uchawi. Hii ni kwa mtazamo wa miaka mingi sana ya watu wenye Imani za uchawi kuwa, wao ni waonaji wa matukio ya mbele, wao wanaweza kuzisoma nyota na kutabiri hali za hewa. hii huitwa ‘’Astrology’’ na ndiyo elimu ya nyota pia, ambayo huaminiwa kuwa ilikuja kuzaa sayansi za anga na nyota ‘’Astronomy’’. wachawi huonekana kuwa wataalamu sana wa maswala ya utabibu, jamii zote zimejaa waganga wa kienyeji kama madaktari. Na hivyo basi, hawa wananukuu kuwa, sayansi za utabibu ‘’medicine’’, ni matokeo ya msaada wa wachawi. pia sanaa za wachawi za uchanganyaji wa kemikali mbalimbali, na kisha kutengeneza madini kadhaa, mfano huweza kuchanganya madini ya ‘’Copper’’ au shaba na kuzalisha dhahabu ‘’gold’’, hii huitwa pia ‘’Alchemy’’, ni msingi mkubwa wa kuzaliwa kwa sayansi ya Chemistry. Uchawi huwepo katika kila tamaduni ya kazi au shughuli za mwanadamu. Hata hivyo kuna shughuli ambazo tangia awali huonekana kuhusiana zaidi na uchawi, kuna Uwindaji, kuna uvuvi, hizi huusisha Imani kubwa sana za ushirikina. Lakini pia kuna shuguli kama za utengenezaji wa vyuma, kuna kilimo, ufugaji, ‘’wachawi hujiita marafiki wa wanyama’’, na zaidi ni maswala ya afya, ambayo uchawi huwa mstari wa mbele sana.
Changamoto kubwa katika mtazamo huu wa uchawi kama mtazamo wa awali kabisa wa kijamii, Ukifuatiwa na dini na kisha sayansi, hauna hoja za nguvu kabisa katika historia, na hata katika udadisi wa kina wa mitazamo ya kijamii ya sasa na zamani. Kwanza kabisa, umeuweka uchawi kama mtazamo wa kijamii, kitu ambacho sio kweli kabisa, wachawi ni wapinzani wa jamii ‘’anti-social’’, wachawi mara zote hukinzana na jamii, wachawi ni watu ambao huwa wakikaa misituni, maeneo yasiyo na watu wengi, Mbali na miji, wachawi huwa hawafanyi shughuli zao wakati wa siku, wao hufanya Usiku, na tena hufanya katika mazingira ya Siri. Wachawi huwa wasiri sana na hufanya vitu ambavyo hukinzana na mapenzi ya jamii zao. Jamii nyingi kwa wastani huwa hawawapendi wachawi tangia zamani hizo za mwanzo wa nukuu za historia. Hakuna kabisa nguvu ya hoja ya kuwa uchawi ni kiunganishi cha sayansi, teknolojia na jamii. una msingi mkubwa kabisa wa kufanya vitu bila kufikiria na hauna kipaumbele chochote cha utafiti.
Uchawi katika jamii zote za binadamu, huusisha sana misingi kadhaa ya utendaji wake, ambao tutauangalia kiundani zaidi. uchawi humwacha mtu huru katika mtazamo wake wa kijamii. Utakuta katika jamii za wakristo kuna wachawi, jamii za kiislamu kuna wachawi, jamii za kihindu, jamii za kibuddha, kwa wapagani, shamanists, Voodoo, wasio na dini kuna wachawi ‘’atheists’’, taasisi za siri zimejaa wachawi ‘’occultists’’ kama freemasons, illuminati , cross and bones’’, Imani za umizimu ‘’spiritualism’’ zimejaa uchawi, n.k. kwanini jamii hizi zote huwa na uchawi, ni kwa kuwa, uchawi ni sanaa ambayo misingi yake huweza kufuatwa na mtu yeyote yule kama tutakavyoiangalia hapo mbele. Historia bora kabisa ya kuuelewa uchawi ni mtazamo uleule bora kabisa, uchawi ni sanaa ambayo imekuwepo tangia awali kabisa katika historia ya mwanadamu. uchawi hupitia kipindi cha kupanda na kushuka, jamii zinapoongeza sana uasi wa Mungu na kimaadili, Uchawi hushamiri sana, na jamii zinapoongeza uchaji kwa Mungu wao, uchawi hupungua.
Uchawi hauna msingi wowote wa elimu ya kweli, ila uchawi una siri kubwa sana za kucheza na akili za watu, kupitia utendaji wa mbinu za kichawi ‘’Magical-Causality’’. Maswali kama Uchawi umewezaje kufanya hivi? Amewezaje kusafiri? Amelogwaje? Kajibadilishaje? Hivi vitu kwa ujumla hufahamika na wachache sana. Uchawi huwa na siri sana ambazo hata wachawi wenyewe hawazijui. ila huwa una nguvu sana za kuathiri jamii za watu, kwa kuwa mbinu zake huwa na nguvu sana katika mitindo ya maisha isiyo ya maadili na maarifa. Katika maktaba kubwa duniani, historia za uchawi zimejaa, lakini nukuu za historia za sayansi za utafiti wa uchawi, zinahesabika kwa idadi ya vidole vya mikono. Wanasayansi wengi sana katika zama za utafiti mkubwa duniani, karne za 17 mpaka 19, hawakuwahi kuona kama kuna haja ya kuwekeza nguvu kuutafiti uchawi. Hii ni Kwa kuwa walijua, uchawi hauna ajenda za msingi sana za kuinufaisha jamii.
Na ni kweli, Baba wa sayansi, Sir Isaac Newton aliwahi kufanya utafiti wa kina katika sayansi za ‘’Alchemy’’, lakini hakuna nukuu yoyote ya msingi aliyowahi igundua. Kama angekuwepo J.G. Frazer leo, akaulizwa unashuhudia uchawi uliosema kuwa ndiyo mtazamo ulikouwepo kabla ya Dini na sayansi, leo ndiyo unateka tena dunia, Uchawi ulioingizwa hata katika sayansi za akili, kwa triki za ‘’Meditations’’, ambazo kadri zinavyotumika kama matibabu ya shida za kiakili ‘’psychotherapy’’, watu wanazidi kuwa wapumbavu wahanga wa Imani hizi ‘’risk groups’’, wasijue asili ya sanaa hizi ambazo ni hatua kadhaa za Imani za kichawi.
Wachawi mara zote katika historia huwa na maadui wao. Na maadui wao ni Wakristo ‘’wakweli’’ na inatambulika kuwa, Biblia tangia awali kabisa, ilikuwa ikiruhusu adhabu kali ya kifo kwa wachawi. Na utaratibu wa adhabu hii uliisha baada ya Kristo kufa msalabani, lakini bado sheria za Biblia, huwataka wachawi kubadilisha Maisha yao, kwa kuwa wamesamehewa bure kwa damu ya Kristo, aliyekufa kwa ajili ya dhambi za kila mwanadamu. Vyombo vingi vya wanahabari wachawi, na hata mitandao ya kijamii ya wachawi, huwa wakitiana nguvu kutojali mitazamo ya wakristo, ambao mara zote huwakosoa. Hoja ni kuwa, Vita hii ilianza muda mrefu sana. Lakini ni muhimu kutambua kuwa, Historia inaonesha kuwa Sayansi ya kisasa imezaliwa mikononi mwa wakristo, na vyuo vikubwa vya awali vyote vilikuwa, na huwa na elimu za dini kama elimu ya msingi. Elimu hii ilihamasisha zaidi Imani za uchawi kuonekana kama namna mbaya zaidi ya kijamii. Na hapa kukazaliwa tatizo kubwa sana kuwahi kutokea, lililoitwa ‘’Witch Trials’’, haya ni mauaji ya wachawi. Karne kadhaa nyuma, wachawi wengi sana waliuwawa, na hasa wanawake, Ambao huonekana zaidi kuhusiana na shughuli za uchawi. Na wengi hawajui kuwa, hata Biblia imeandika ‘’usimwache mwanamke mchawi kuishi’’, ijapokuwa wengi hawajui maana ya agizo hili, lakini mpaka tutakapo maliza sura hii, itatambulika kwanini wanawake huwa hatarini zaidi kwa Imani za uchawi kisayansi. Mauaji ya kichawi yana sababu nyingi sana, lakini hoja ni kuwa, yaliongeza presha kwa wachawi katika jamii kwa kipindi Fulani nyuma, ila sasa uchawi na matawi yake unaendelea kumea kama mmea.
Sanaa Za Uchawi
Uchawi Pamoja na aina zake mbalimbali, bado kuna sifa kadhaa za asili na sifa za kutengeneza, za kuutambulisha uchawi. na hizi huunda tabia za sanaa hizi za uchawi. Kwa kurejelea kazi nzuri iliyokwisha fanywa na Prof-Levi Strauss, sifa hizi husomwa kirahisi baada ya kugawanywa katika makundi kadhaa.
Wachawi
(wachawi, waganga, wanamazingaombwe, wataalamu, n.k)
Wachawi hutambulika kama watu wenye nguvu za ziada ‘’superhuman powers’’. Wachawi huwepo wa aina mbili, kuna ambao husemwa kuwa wananguvu za Ziada za kuzaliwa nazo, na kuna ambao husemwa kuwa, nguvu zao wamekuja kuzipata baadae. na hii ndiyo sababu katika jamii baadhi, husemwa kuwa, baadhi ya watu tangia wakiwa watoto, wana nguvu za kuzaliwa na walipaswa kuwa waganga, hata kama hawataki. Wachawi huwa ni watu wenye nguvu ambazo, baadhi yao huzinunua. nimekuwa nikijua baadhi ya maeneo wanapouza mapembe ya uchawi. baadhi huazima, baadhi huzimiliki ‘’possess’’, n.k. Wanasoshiolojia ‘’socialogists’’ na wanasaikolojia katika elimu hizi, hukubaliana kuwa, Wachawi katika jamii, huwa na sifa kadhaa za kuwatambulisha. hizi sifa zinatokana na mitazamo ya zamani, na ya sasa pia. Sifa hizi sio kila mchawi huwa nazo, lakini huaminiwa kuchochea zaidi ufanisi wa sanaa za ‘’magic’’, yaani uchawi, uganga, mazingaombwe, na zinginezo za mtindo huu
Kiini macho ‘’evil eye’. Sehemu ya jicho ‘’Iris’’ ambayo huonekana kuzunguka kidoti cha kati katika mwonekano wa nje wa jicho, huwa kimemezwa sana na sehemu ya kati yenyewe inayoitwa ‘’pupil’’. Hii humpelekea kuwa na utazamaji wa tofauti kidogo, husemwa pia kuwa jicho lake limekosa kivuli. Msisimko mkubwa ‘’hyper-sensitive’. Wachawi wengi sana huwa na sifa za kuwehuka, kitaalamu huitwa ‘’Hysterical’’. hii inahusisha tabia ya kuhemka hemka kirahisi sana. Jambo dogo kwa mchawi humfanya kusisimka sana. Katika dunia kote wapo wale wenye mionekano ya kutoaminika ‘’cunning look and untrustworthy’’, wachawi huwa na sifa ya kuangalia kitu kwa kukazia sana Jicho au macho ‘’blink strangely’’, hii tabia ya kuangalia kwa kukazia macho, ni misingi ya training za uchawi, wao huita ‘’visualization’’. na hizi zote hujumuishwa kwenye msemo uitwao ‘’kiini macho’’ ambapo kwa Kiingereza huitwa au ‘’evil eye’’. Mchawi hufundishwa kujiuliza kwa kila kitu ‘’question everything’’, mchawi hujifunza kuzingatia sana mabadiliko hata madogo sana katika mazingira yake, unaweza sema ni watu walio na hisia za juu sana katika uchukuaji wa taarifa zinazowazunguka ‘’highly sensitive’’.
Jamii nyingi zimekuwa na utambulisho wa wachawi kama watu ambao akili zao hazipo sawa sana ‘’nervous’’. Au watu wenye shida kidogo za kiakili ‘’sub-normal people’’. Hata mtu akirukwa na akili tu ghafla, watu huarakisha kuamini kuwa amerogwa. Na hii ni mitazamo iliyoshamiri sana katika maeneo yaliyo nyuma kielimu . Wachawi hutambulishwa pia kama watu wenye mikao, mionekano na namna za kuwasiliana za vitisho ‘’violent gestures’’, huwa na sauti za kukwaruza na kuunguruma kwa baadhi ‘’, huwa na vipaji vya kutunga mashairi ‘’poetic gifts’’. Sifa hizi mara nyingi huambatana na waganga wa kienyeji kwa maeneo mengi sana. Nyingi ya sifa zao huunganishwa katika sifa za tabia za kutokuwa sawa kiakili, Au ‘’nervous signs’’. Na sifa hizi mara nyingi sana huoneshwa pindi ya matamasha yao. Sifa hizi kitaalamu huweza wekwa kwenye makundi matatu yaani ‘’nervous trances, hysterical crisis and cataleptic fits’’. Hizi ni jumla ya sifa zote za juu, yaani, kutokuwa na utulivu wa kina wa kiakili, tabia za kuwehuka na kuripuka, na tabia za kutumia macho kwenye ajenda zao.
Wachawi huingia katika hali ya hisia kubwa za raha ‘’ecstacy’’, ambazo mara nyingi huzipitia kwa asili au hujitengenezea mazingira hayo. Tabia hizi utazigundua kwa baadhi ya wachawi kupitia matumizi ya ‘’Spell’’, hizi tamaduni huwa na michanganyiko ya kemikali mbalimbali za mimea na baadhi ya vitu, na kisha huvinenea kutaka matakwa yao, huwa katika namna ya kujivukiza. katika hii hatua hujisikia misisimko mikubwa sana ya kihisia, na hapa huwa mithili ya waliopoteza fahamu, hujiona wakiwa katika ulimwengu wa mbali sana na dunia. hizi ‘’spell’’ zimejaa katika tamaduni za wachawi, wakifundishana namna ya kuchagua, kutengeneza na hata kutumia, na pia hufanya wanapokuwa Pamoja. Kumbuka spell haifanywi kwa jamii zote, ila hufanywa kwa aina zao. Sifa za kuweza kuburudishwa na tamaduni hizi kiakili, hutambulishwa kama bahati ya uwezo wa asili wa kuzungumza na miungu ‘’Spiritual gifts’’. Na hii huwafanya kukidhi kuwa wasanii wa magic au wachawi au waganga. Na hasa inapoambatana na sifa kadhaa za nje tulizokwisha ziona.
Wanawake na Uchawi. Wanawake huonekana kuwa mbeleni sana katika sanaa za kichawi. Na inatambulika hii ni kulingana na vipindi mbalimbali vya mzunguko wa Maisha yao. Vipindi Hivi huonekana kuwaweka kwenye nafasi nzuri zaidi wanapojihusisha na sanaa za kichawi. Na hasa ni vipindi vya kuvunja ungo, hedhi, ujauzito na uzazi wa Watoto. vipindi hivi huusiana na uhitaji mkubwa sana wa wanawake katika sanaa za uchawi. Wanawake wazee huonekana kama wachawi, mabinti Mabikra huonekana kuwa na thamani sana katika uchawi, damu za hedhi huitajika sana katika uchawi, na pia yapo mengi yanayohitajika katika uchawi toka kwa wanawake.
Wanasosholojia huitimisha kuwa, wanawake pia wapo hatarini sana kupatwa na shida za mihemko ya kuwehuka ‘’hysterical’’’ na changamoto za kiakili ‘’nervous crisis’’, kumbuka pia , katika sehemu ya nne tuliona kuwa, wanawake wapo hatarini zaidi kupatwa na changamoto za kiakili za shida za kihisia, kutokana na utumiaji wao bora sana wa mfumo wa ubongo, wa ‘’mirror neuron system’’ , wanawake wanauwezo mkubwa zaidi wa kutazama na kuvuta taswira ‘’gazing and visualizing’’ na pia wanawake wanaathiriwa zaidi na hofu kwa kutoweza kutumia vizuri mfumo wa ubongo, tuliouita TPJ. na hata mfumo wa uharaka wa kupambana na shida au‘’fight-flight reactions’’, na hivyo huwa waoga sana. sifa hizi huwafanya wanawake kuwa hatarini zaidi au kuwa na mafanikio zaidi katika nguvu za giza.
Wachawi katika upande mwingine huwa ni watu wenye maarifa mapana ya asili, na mara nyingi huamini kuwa miungu ‘’gods’’ huwa katika raha muda wote, na binadamu muda wote huwepo katika hali za shida. hivyo kwa kuwa wao huwepo Katikati ya miungu na binadamu ‘’mediators’���, basi huwa katika nafasi nzuri sana ya kunufaika. wachawi huamini kuwa huwa na zawadi ya kuambiwa mambo mengi zaidi ya watu wa kawaida kupitia kuwasiliana na miungu. na zaidi kabisa, ni Imani ya uwezo wao juu ya vitu.
Kuwanga na Kupaa ‘’Power of Levitation’’. Wachawi huaminiwa kuwa na uwezo wa kuwanga, Na kupaa. Huu uwezo huwawezesha kufanya vitu bila kuathiriwa na kani ya mvuto wa gravity, ana uwezo wa kusafiri na kuwa popote kwa wakati wowote ule. Mchawi katika wakati mmoja huaminiwa kuweza kuwepo zaidi ya eneo moja. Yeye habanwi na sheria za kupaswa kuwa eneo moja ‘’laws of contradiction’’. Ilirekodiwa katika historia mwaka 1221, bwana Johannes Tentonians wa Halber’s tadt, mhubiri na mshirikina ‘’sorcerer’’, alionekana kuhutubia makundi matatu yaliyo mbali mbali, kwa wakati mmoja, Moja ikiwa Halberstadt, lingine Mainz, na lingine Colign. Asili ya miondoko hii ya wachawi bado haifahamiki ‘’uncertain’’ kwa wanasoshiolojia, hasa kama wachawi hawa huondoka wao wenyewe, au sehemu yao, au lah. Na ni wanateolojia na wanafalsafa tu ambao walionesha sana tangia awali kulifuatilia hili kiundani.
Mwili na Roho ya Mchawi. Kitendawili kimerejea tena katika sosholojia ya kujifunza uchawi. Na hii ni kwa kuwa, roho ya mchawi hupelekea maswali mengi sana kwa wasomi hawa. Roho ya mchawi huonesha kuwa na siri nyingi za kishirikina ‘’occultic qualities’’. Huaminiwa kuwa roho ya mchawi huwa inaelea elea ‘’mobile’’ , na huwa ikifanya hivyo kulingana na maamuzi ya mchawi mwenyewe. Huaminiwa kuwa roho yake huweza kujitenganisha toka mwili wake. Na hizi namna ambazo huitwa ‘’levitation’’, zimeshamiri zaidi katika tamaduni za kichawi za ‘’Shamanism’’ na ndiyo msingi mkubwa zaidi. Roho ya mchawi huonekana kuwa ni sehemu ya pili ya mchawi mwenyewe, yaani ni ‘’Double’’ yake mwenyewe. Na sehemu yake hii huonekana kuwa imeungana na yeye mwenyewe mchawi, na inaweza safirishwa kuelekea popote pale kwa maamuzi binafsi ya mchawi. Na kikubwa zaidi ni kuwa, roho yake hii anayoiamuru, huweza kufanya vitu popote katika ulimwengu wa kawaida kabisa, na sio wa kiroho. Kwa baadhi ya mazingira huoneshwa kana kama mchawi mwenyewe, anaweza Jigawanya ‘’Split’’ katika namna mbili. Mfano imewahi rekodiwa kwa mchawi ‘’Dayak’’ aliejigawanya sehemu moja ikienda kutafuta dawa, na nyingine ikihudhuria ibada. Watu huuona mwili wa mchawi lakini yeye kiroho hayupo pale.
Huonekana kuwa hii roho yake nyingine, au sehemu yake nyingine, huwa ikishirikiana kwa kubadilishana na mwili wake, yaani yeye huwa anaamua awepo wapi. Anapoamua kuwepo, ndipo yeye wa uhalisia huwepo, na sehemu ya nyingine, huacha tu mwonekano wake. Mtindo huu umeonekana kuhusika kwa wachawi wa ‘uvvgnn, hawa walikuwa wakisema kuwa mchawi ameudhuria sabato, na mwili wake uliobaki kitandani ni pepo, Au ‘’vicarium daemonem’’. Na huyu pepo aliyebaki, ndiye asemwaye kama sehemu yake, au ‘’his double’’. kubwa zaidi pia ni kuwa, sehemu ya pili ya mchawi, huwa ikielea mithili ya kitu, mfano wa pumzi, spell ni formula zake za kipindi cha kuanza kuingia katika ibada za kuwanga, ambazo huwa akizinenea kwa kuelekeza akili zake huko. sehemu hii ya pili ya mchawi au pepo lake, inaweza mwingia mtu yeyote yule, Na huweza kumwingia bila hata ridhaa yake. Na mtu huyu hujikuta tu akiwa mtendaji wa matakwa ya mchawi mwenyewe. Safari ya Wachawi huonekana kutokuwa peke yao, huwa na wasaidizi wao ambao ni sehemu yao ya pili ‘’their double’’, na roho zingine ‘’spirits’’ za namna ya pepo ‘’external souls’’.
Mchawi na Kujibadilisha Maumbo ‘’Metarmophosis’’. Kujibadilisha maumbile kwa wachawi ‘’shape changing’’ huusisha wachawi kujibadilisha na kuwa viumbe. Kwa Ulaya ‘’Europe’’ iliaminika hii kuwa ni mbinu ya wachawi kusafiri kwa anga, wanapojibadilisha kuwa ndege ‘’aerial flight’’ katika zama za kati ‘’Middle Ages’’, katika Rumi ya Kigiriki, Bundi ‘’Strix’’ ambaye alikuwa na hali zote, yaani ndege na pia ni mchawi, Alitambulika kama mwanamke mchawi,na pia alitambulika kama paka mweusi aliyekuwa akikaa pembeni mwa nyumba yake. Na hii iliambatana na falsafa ya kuwa, mchawi anapokuwa akifanya ubaya, huwa akiivaa hali yake ya unyama . Na iliaminiwa kuwa mwanamke huyu mchawi anaporuka usiku akisafiri, Huongozana au huambatana na sehemu yake ya pili ‘’double’’ yake, na mnyama wake. Ambaye kwa wakati huu, huwa sio katika hali ya mchawi, bali huwa kama familia yake.
Hii ilikuwa maarufu sana kwa kesi ya Paka mmoja maarufu aliyeitwa ‘’Rutlerkin’’ aliyekuwa akimilikiwa na mchawi ‘’Margareth na Filippaflower’’, ambao hawa walichomwa wote kwa Pamoja mnamo tarehe 11 mwezi wa tatu, mwaka 1619, kwa kesi ya kumuwangia ndugu wa Mfalme wa Rutland.Wanyama ni ajenda kubwa sana katika Imani za kichawi kuliko wengi wanavyohisi. Ni kama kile kielelezo cha shetani kumtumia Nyoka kwa eva. Hoja za mfanano huu ni nyingi sana katika Imani za mazingaombwe.
Uwezo wa Kuzungumza na Roho za mapepo na wafu ‘’Spirits’’. Uwezo wa kujitenga kimwili wa mchawi na kuzungumza na roho za mapepo au miungu ‘’spirits’’, hutofautiana kwa viwango baina ya wachawi. Wachawi hujua maeneo ya roho hizi zinapopatikana. Hutambua namna ya kuwasiliana nazo, hutambua pia namna ya kukutana nazo kupitia namna zao za ibada. Na pia huamini kuweza kuwasiliana na roho za waliokwisha kufariki. Ni rahisi sana kwa waganga kusema kuwa wameongea na waliokufa. Katika visiwa vya Melanesia, huaminiwa kuwa wachawi hupokea nguvu toka kwa roho za ndugu zao wa damu waliokufa. Undugu wa damu huaminiwa kuwa ni msingi mkubwa wa uhusiano kati ya mchawi na roho.
Mapepo ya Mapenzi ‘’Succubus and Incubus’’. Wachawi katika historia wamewahi tambulishwa wakiwa na mahusiano na mapepo ya mahaba. Ambapo incubus huwa ni pepo linalolala na wanawake wanapokuwa wamelala, na hivyo hivyo kwa wanaume huwa succubus. Imani hizi zote huambatana na wachawi kuonekana kama wasanii wa kupenda mitindo ya uchafu wa kimapenzi ‘’lascivious’’. Na pia wanawake wa kichawi walikuwa wakifahamika kwa sifa hiyo hiyo, ambapo kwa zamani walikuwa wakitenda kama wanawake wa sifa kubwa katika jamii, wenye wapambe wengi, na walikuwa wakikutana na wanaume wenye utajiri au mali nyingi.
Kuwa na Mapepo ‘’Possesion’’. Hutambuliwa pia kuwa Wachawi huwa na mapepo kichwani mwao. Na wao pia hutambua kuwa wanayo vichwani mwao mapepo yanayowaendesha, japokuwa huwa na uwezo wa kuchangamana nayo. Katika uchawi wa ‘’Shamanism’’ tutakao angalia misingi yake mbele kidogo, kumilikiwa na mapepo au ‘’spirits’’ ni msingi mkubwa sana wa Imani ya kichawi. Na kwa ujumla kwa wote, hutambulika kuwa na mapepo ‘’spirits’’, ndiyo msingi bora zaidi wa kichawi. Mchawi anapokuwa ana pepo, Sio tu kuwa anahisi uwepo wa mtu mwingine ndani yake, Lakini hata utu wake ‘’Personality’’ huwa ni matokeo ya pepo ‘’demon’’ lililo ndani yake. Na ni hili pepo lililo ndani yake ndilo humfanya atamke maneno katika mdomo wake. Na hapa hutengeneza mjadala mwingine wa matokeo ya kisaikolojia na kifiziolojia, unaohusiana na mabadiliko ya tabia ya utu wa mtu. Mchawi huweza kutawala kumilikiwa na pepo lake, kupitia kufanya baadhi ya matendo. Na matendo haya hasa, huwa ni kucheza muziki wa sauti zisizopishana pishana sana, unaojirudia rudia, huitwa pia ‘’Monotonous music’’, lakini pia, kupitia michanganyo baadhi ya kujivukiza akili zake. Utaalamu ‘’Professional’’ wa mchawi sio kuwa na maarifa mengi, lakini ni uzoefu mkubwa wa kutumikia nguvu zake, au kumilikiwa ‘’possesed’’, hii humfanya kuwa mtaalamu zaidi.
Kumkaribisha Mchawi Mpya ‘’Initiation ceremony’’. Hii huwa ni hatua ya lazima ya kila mchawi anayepitishwa rasmi kuwa mchawi. Huusisha viapo, ibada mbalimbali za matendo zinazolenga kuonesha kuwa, sasa anavuka kizingiti Fulani, na kuingia katika hatua mpya. Hapa sasa huanza kuambiwa hata elimu pana zaidi za siri. Mara nyingi ibada huongozwa na kiongozi mkubwa wa jumuiya ya kichawi ‘’Coven’’. Hatua hii huusiana na ongezeko kubwa la nidhamu, pia hisia za motisha kwa mchawi mpya. Na kwa tamaduni za mashariki, huonekana kuambatana na ongezeko kubwa la nguvu za ziada, au ‘’supernatural powers’’ ziitwazo ‘’siddhi’’ au ‘’sutra of patanjali’’, nguvu hizi hupatikana pia kupitia mitindo ya ‘’meditations’’ katika tamaduni za Yoga kwa wabuddha.
Hatua hizi kwa baadhi huusiana na mchawi mpya Kwenda kulala katika kaburi la bibi mzee, wakati wa usiku, na hatua zingine nyingi. Na baada ya hatua hizo, husafirishwa mpaka katika kilele cha mawingu, huonana na miungu na roho za mapepo ‘’spirits’’, akili zake zinapomrudi anapokuwa ameamka, hujikuta akizungukwa na vitu mbalimbali kama madini baadhi ‘’quartz’’, madawa, na vinginevyo vingi kwa ajili ya utu wake mpya. Pia huwepo tamaduni za kichawi ‘’rituals’’ za kuvirasimisha vitu baadhi, na hata maeneo kwa shughuli za kichawi, hizi huitwa ‘’consecration’’, hutengeneza mazingira maalumu kwa shughuli za kichawi. Huaminiwa kuwa hii hatua huusiana na kupita katika kifo cha muda mfupi ‘’temporary death’’ na baada ya hapo, mtu huwa akiingia katika ulimwengu mpya. Na hapa katika kipindi cha kifo cha muda mfupi, kama kielelezo cha ubatizo wa wakristo, mchawi hufunzwa namna za kutumikia nguvu zake au kuhusiana na mapepo yake.
Kiini Cha Nguvu Za Uchawi ‘’Magical Powers’’. Nguvu za kichawi zote zimejengwa katika msingi mkuu mmoja, ambao ni wa kujitenganisha kati ya mwili na Roho. Katika uchawi wa ‘’Shamanism’’, kujitenganisha kwa Roho toka mwili au ‘’separation of body and soul’’, na kumilikiwa na mapepo ‘’possesion’’, ndiyo misingi mikubwa zaidi, kama ilivyo pia kwa jamii zote za kichawi. Na msomaji anapaswa kulielewa hili.
Miiko Ya Wachawi. Wachawi kuifikia nguvu kubwa ya kichawi, hupaswa kuwa na mitindo mbalimbali ya kimaisha. Hasa kurudia rudia mawasiliano na roho za mapepo, kupitia ‘’kumilikiwa’’ au ‘’possesion’’. Na hapa hufanikiwa kupitia kujenga nidhamu kubwa sana kupitia matendo kama, kujizuia na baadhi ya vyakula ‘’wachawi huwa hawapendi kabisa kula baadhi ya vyakula’’, huogopa kuondoa uhusiano mzuri na mapepo yao. pia huelekeza Maisha yao katika mazingira ya misituni au maporini. hulala makaburini mazingira Fulani, Wachawi pia huwa na miiko mingi sana au ‘’Taboos’’, hujizuia kufanya baadhi ya vitu, lengo huwa kuulinda uhusiano wao na mapepo yao.
Hisia Kuu za Raha kwa Wachawi. Ni muhimu kutambua kuwa, wachawi kwa kulinda uhusiano wao na mapepo yao, hujikuta wakiwa katika hali ya juu sana ya raha inayoitwa ‘’ecstacy’’. Hali hii huusiana na kutokuwa na hisia za kimwili za kawaida, hali hii huitwa ‘’altered states of consciousness’’, na hapa mchawi hujiona akiwa katika uwepo wa mbali zaidi. Hali hii hufikiwa kupitia kucheza ngoma, kuimba nyimbo za kujirudiarudia na biti za ufundi maalumu ‘’chanting’’, kwa kucheza, na kupitia kuvuta taswira‘’meditation’’. Hisia hizi za wachawi huusiana na uhusiano na miungu, Pamoja na roho za mapepo, unaweza uita pia kama ‘’Mystical union’’, wachawi hujiona wakiwa Pamoja na nguvu za giza, hujiona wakiwa Pamoja na uwepo wa mungu ‘’kuna msemo husemwa, kwa Mungu kuna raha’’, wachawi pia hujiona wakizidishiwa nguvu ‘’magical empowerment’’. na hapa ndipo hujihisi pia wakipatwa na hisia za usanii wa ujenzi na alama ‘’Symbolism’’. hisia hizi hulenga kutengeneza alama za miungu yao, ambazo wanapoziona huwafanya kujisikia hisia za kuwa karibu na miungu yao. Wachawi hujihisi kuwa na hisia za uwepo wa nguvu kubwa ndani yao ‘’transcendence’’. ambazo huwafanya kuhitaji zaidi kujiweka karibu na miungu yao na kujitakasa kwa watakayopaswa kuyafanya. Uwezo wao wa kutenda kimiujiza huongezeka wanapokuwa katika hali hii.
Wachawi na sanaa za uchoraji na ujenzi. Wengi wasiolijua hili, huwa hawaelewi kwanini wachawi wengi sana hupenda sana sanaa za uchoraji ‘’drawing’’, kupakapaka rangi michoro au ‘’Painting’’, hupenda pia ‘’Carpentry, na construction duties kwa ujumla’’, hata neo ‘’Crafts’’ katika ‘’Witchcrafts’’ humaanisha ni sanaa, kuna wengine hujiita ‘’masons’’ au ‘’Freemasons’’, hawa nao hujiita wajenzi. Kuna makundi mawili ya uchawi, kubwa zaidi huwa halina matumizi ya maneno sana, hutumia sana alama, na huitwa ‘’non-verbal’’, hupenda kuchora sana tattoos za miungu yao, huvaa chain za miungu yao, majengo yao huyajenga kwa design na picha za miungu yao, n.k. Usipokuwa makini, Unaweza shindwa elewa kwanini hawa watu wanawapenda sana miungu yao. Ni kutokana na hisia hizi ambazo huwa wanazipata wanapokuwa na miungu yao. Usipokuwa makini hutaelewa hata kwanini, wabuddha na wahindu, hufumba macho masaa na masaa wakivuta taswira kupitia ‘’meditation’’, Jamii hizi nyingi utaona tamaduni hizi, wakifumba macho, wakacheza miziki kwa steps usizozielewa huku wakiburudika sana. Msingi ni uleule, Hakuna binadamu anayeweza kuvutiwa kufanya kitu, kama hakimpi msisimko mkubwa.
Matendo Ya Wachawi
Sehemu kubwa tumekwisha iona kupitia msaada mkubwa wa elimu ya sosholojia ya namna wachawi wanavyotenda. Matendo mengi ya wachawi huwa yana maelekezo ambayo huwa hayana msingi maalumu wa utendaji, bali hutegemeana kati ya mtu na mtu, au mtu na kikundi. Mfano, uelekeo wa kuangalia kwa mchawi una maana kubwa sana. Wachawi huwa na sabato zao, ambazo huwa siku za ijumaa. hizi kwao huwa na maana kubwa sana.
Wachawi huzingatia sana mizunguko ya mwezi, na hii ndiyo sababu ya elimu za nyota kushamiri katika sanaa za kichawi ‘’astrology’’. Wachawi huzingatia sana siku, mfano ambazo jua huwa mbali sana na equator ‘’solstitial days’’ mfano tarehe 21 mwezi wa sita, na pia tarehe 21 mwezi wa kumi na mbili, pia hujali sana ule usiku kabla ya hizi siku, na huuita ‘’solstitial eves’’, hujali pia siku ambazo muda wa usiku na mchana huwa sawa ‘’equinoctial days’’ mfano, tarehe 23 mwezi wa tatu, na pia tarehe 23 mwezi wa tisa. pia huzingatia zile siku za ziada katika kubalansi urefu wa miaka ‘’intercalary days’’, mara nyingi siku hizi huwa ni za muhimu sana kwa ajili ya sherehe za kichawi. Na pia huongoza taratibu zao za ibada zao za kichawi. Inashangaza pia kuwa, tarehe nyingi sana za sherehe kubwa za watakatifu wa kikristo wa katoloki, ikiwemo na sherehe ya christ-mass, huambatana na tarehe za matendo mengi sana makubwa katika ibada na sherehe za kichawi.
Maeneo ya mikutano ya wachawi. Uchawi hufanyika sana katika maeneo ya makutano ya Barabara, makaburini, katika misitu, pembezoni mwa miji, kwenye mashimo ya uchafu, na maeneo haya huaminiwa kuwa, huwa na mapepo sana. Wachawi wanapokuwa wanalenga kuroga sehemu Fulani au kuiingia, hufanya kuanza kuizingira, Kwa kutengeneza mduara kuizunguka.
Wachawi na mabaki ya Vitu. Wachawi huchuma mimea kadhaa kwa kutumia vidole maalumu tu kwa ajili ya ibada zao. Wachawi pia hutumia sana vitu vingi kama uchafu, nywele nywele zilizobakia baada ya watu kunyoa, mabaki ya miili ya Watoto waliokufa kipindi cha kujifungua, uchafu wa nyumba za watu, hutumia uchafu mwingi sana ambao hudharauliwa katika jamii. Wachawi huwa na michanganyo kadhaa ambayo huitumia kugundika michanganyo yao, kama vile hutumia asali, maji, nta, maziwa, n.k. na hutumia toka kwa Wanyama wenye sifa maalumu tu, kama vile rangi, jinsia, umri na hata maumbile. Michanganyo hii huitwa pia ‘’Magical pharmacopoeia’’.
Wachawi na Kafara. Wachawi pia huegema sana katika ibada zenye mitindo ya kafara. ambazo huambatana pia na matumizi ya alama mbalimbali, kulenga matendo kwa ajili ya miungu yao. Lengo kubwa la kafara ni saikolojia ya Ubongo. unapotoa kitu, akili yako huwepo pale. Ukimgharamia sana mwanamke, akili yako itakuwa pale. Biblia imeandika, ‘’ilipo hazina yako, ndipo ulipo moyo wako” ukitoa zaidi sehemu yako, hata kama itakuumiza, ndipo moyo au akili yako itajikita zaidi au unajitoa zaidi. Ibrahimu alipomtoa Isaka, au Mungu Baba alipomtoa mwanawake wa pekee, Kielelezo hiki kinalenga kukuonesha nini kilikuwa nyuma ya mioyo yao. wachawi hutoa kafara pia kukazia maagano yao. ili Pepo limmiliki zaidi mchawi, inapaswa akili yake ijitoe zaidi. Usipojua hili unaweza hisi wenda Mapepo Yanataka Damu, Hapana. Hizi huwa ni lugha za vielelezo au alama ‘’symbolic’’, hata Mungu pia haitaji sadaka, kwa kuwa yeye ni Tajiri tayari, ila utoaji wa mtoto wake ni kielelezo tu cha kuonesha ulipo moyo wake, ni kwa Mungu wake.
Wachawi hutoa kafara za wale wanaowapenda, ambao hunukuliwa zaidi kuwa ni watu wao wakaribu, hasa kwa uhusiano wa damu, kama vile Watoto. Lakini lengo hasa huwa, kwakuwa ndugu wa damu kuwatoa itamuuma sana mchawi akitoa, Pamoja na kuteseka sana kihisia, lakini mwishowe, akili yake itamezwa zaidi katika kuwa mfuasi mkubwa wa uchawi. Wachawi huandaa taswira toka michanganyo mbalimbali, ambayo haina umuhimu katika hii sehemu. Wachawi hutengeneza rangirangi za ajabu, pia hujipaka, urembo na mikufu ya kujifunga, ikiwemo na irizi. Mara nyingi hufanya hivi kuwasilisha vielelezo vya mapepo yao.
To be continued...
Mwandishi na Mwenyekiti
Mtaalamu wa sayansi ya wanyama, mwanabiofizikia, na mwandishi wa vitabu vya kisayansi. Mwanzilishi wa Injili ya Sayansi — taasisi inayounganisha maarifa ya kisayansi na imani.
Shiriki makala hii
13 min
3 min
4 min